Utangulizi: Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika Mashariki

“Our landscape is its own monument: its meaning can only be traced on the underside. It is all history.” (11) Edouard Glissant. Caribbean Discourse: Selected Essays

Historia ya Jamii Yangu

Utotoni, sikuisha kushangaa jinsi familia yangu ilivyo ambatanisha sehemu mbali mbali na historia ya mababu. Kitamaduni, sisi tulikuwa Wakikuyu. Nguzo zetu ziliibuka kwenye ardhi yenye rotuba huko Mlima Kenya, miteremko ya Aberdare, na wilaya za Kiambu na Kikuyu. Hili halikunistaajabisha. Sawia, makabila mengine yalikuwa na nguzo zao tofauti tofauti: kwa mfano jamii ya Wadholuo kando ya Ziwa Victoria (Nam Lolwe), jamii ya Waluyha katika sehemu za Kakamega na Vihiga, nao Wamasai kwenye malisho ya Bonde la Ufa.

Hata hivyo, hadithi hizi zilitatanisha lengo la kuunganisha makaazi na kiini cha kila jamii. Mababu wake baba, kwa mfano, hata ingawa walijitambulisha kama Wakikuyu, walikuwa wamechanganyika na kuoana na Wandorobo—wakaazi wa jadi huko Mlima Kenya waliowatangulia Wakikuyu katika sehemu hizi. Mwanzoni mwa karne ya ishirini, babu Mariibe, na mwanawe Karũgũ, walihamisha mifugo kutoka Gachie hadi Waithaka. Baada ya kumfanyia kazi mwandishi wa Kiingereza Karen Blixen, walihamia Gĩkambura miaka ya Thelathini. Babu yangu na babangu huashiria Gĩkambura kama mahala pao pa utotoni. Lakini sikufahamu kabisa mbona wakaamua kuisahau historia ya jamaa wao kabla ya kuwasili Gĩkambura. Yaani, kwa nini hawakuzikusanya safari zao Mariibe na Karũgũ katika kumbukumbu za familia?

Ukoo wake mama, vile vile, unayo historia iliyoshushia nanga sehemu kadha wa kadha. Wahu, mama yake nyanya, alikulia Rirũta, akasomea Thogoto, na kisha akawa muuguzi katika hospitali ya Scottish Church Missionary. Alikuwa mmoja wa watoto wengi wa aliyekuwa Paramount Chief Kĩnyanjui wa Gathirimũ. Wahu pamoja na bwanake waliishi Nairobi, na baada ya kustaafu wakajenga nyumba yao Gĩkambura. Msichana wao wa kwanza, nyanyangu Wanjirũ, alisomea shule ya Manguo, takriban miaka mitano kabla ya mwandishi Ngũgĩ wa Thiong'o kujiunga na shule hiyo hiyo. Hatimaye, Wanjirũ alifanya kazi mjini Nairobi—katika hospitali ya King George (Kenyatta National Hospital) na kwenye shirika la wafanya kazi la Transport & Allied Workers—kabla ya kustaafu na kuelekea sehemu za Juja—nyika iliyoko kaskazini mashariki mwa Nairobi. Mimi mwenyewe, utotoni nililelewa Gĩkambura, wazazi wangu walipokuwa wakianzisha boma yao, kabla ya kuhamia Ngong. Ngong imo katikati ya sehemu walipokaa Wakikuyu na Wamasai kwa muda wa karne nyingi. Sehemu hii imehimiza na kuendeleza juhudi za ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji ambao wamekuwa majirani, mashemeji, na washirika wa pamoja katika biashara.

Kati ya mikoa yote ambayo familia yangu imepata kuishi, aidha kando ya Wandorobo wa Mlima Kenya, katika jiji la Nairobi, kwenye mashamba ya Rirũta na Thogoto, hadi kwenye nyika za Juja, kunaibuka historia nzito na kumbukumbu nyeti. Hii ni juu ya mabadiliko makuu ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa yaliyoambatanishwa na ukoloni wa Mwingereza hadi utawala wa serikali ya Jamhuri ya Kenya. Wakati huo huo, kila sehemu—Gachie, Waithaka, Gĩkambura, Rirũta, Thogoto, Nairobi, Manguo, Juja, na Ngong—inaashiria ugumu wa kufuatilia ukabila kati ya vizazi kadhaa. Kwenye heka heka za kisiasa duniani, ushirikiano wa kijamii, na uhamiaji, jinsi wazee wangu walivyojaribu kuishi ndivyo jamii zingine—sio tu za Afrika Mashariki, lakini hata za bara nzima—zilivyojimudu kimaisha. Maamuzi yaliyojiri yalikuwa kuasi, kushirikiana na mabeberu, kujiunga na shule, kufanya vibarua, kuingilia dini la Kikristo, kuoa, na mengine mengi.

Swali ni, vizazi hivi vinne viliashiriaje topografia ya mazingira yao? Lugha ya Kikuyu inayo majina kadha ya kuzungumzia ardhi na mandhari: ituamba, mĩtitũ, rũrie, werũ, na gĩthaka. Zaidi ya hapo, walivyozidi kujifunza lugha ya taifa, wahenga hawa waliyatumia majina kama vile milima, nyika, jangwa, na chemi chemi. Kuashiria tofauti kati ya matumizi ya ardhi, Kiswahili pia huzungumzia juu ya kichaka, shamba, msitu, na mbuga. Kila jina linaonyesha matumizi ya kipekee na linabeba filosofia maalum kuhusu mandhari yanayopendeza, maadili ya kijamii au kibinafsi, na thamani iliyopo ardhini. Kikuyu na Kiswahili siyo lugha za kipekee katika suala la kuashiria na kuzungumzia ardhi au mandhari. Lugha ya Kikamba ina uwezo huo huo. Katika makala yake “Breathing Life into Dead Theories about Property Rights in Rural Africa,” Celestine Nyamu-Musembi anatofautisha kati ya maneno matano ambayo huashiria hali kadha za ardhi: weu, kisesi, kithaka, muunda, na ng’undu. Kwa vile Kikuyu, Kiswahili, na Kikamba ni lugha za Kibantu, maneno haya yanaambatana katika lugha hizi tatu. Kwa mfano, kithaka, gĩthaka, na kichaka yote yana maana ya ardhi ambayo imejaa magugu, nyasi, na ambayo haijapata kuchimbwa wala kulimwa. Hivyo basi, sio ajabu kwamba maneno haya yana matamshi yanayofanana.

Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika

Jinsi lugha za Kikuyu, Kiswahili, na Kikamba zinavyoashiria ardhi na mandhari kunajitokeza pia katika fasihi ya Afrika Mashariki iliyoandikwa kwa Kiingereza. Kwa mfano, mwandishi Ngũgĩ wa Thiong’o amechapisha vitabu kwa lugha za Kikuyu, Kiswahili, na hata Kiingereza. Yvonne Owuor amezichanganya sanaa za ardhi kutoka jamii ya Waturkana kwenye riwaya yake, Dust (2014). Mashairi yake Okot p’Bitek, Song of Lawino (1966) na Song of Ocol (1967) yaliazima kwa njia kuu jinsi lugha ya Kiacholi huashiria mandhari na jinsi watu wa jamii hii wameyatunza mazingira yao. Mwishowe, mshairi wa karne ya kumi na tisa, Mwana Kupona binti Msham, aliyategemea malezi yake ya Kibantu na ya Kiarabu katika kutunga “Shairi la Binti Kupona.” Cha kweli ni kwamba, mithili ya ardhi na mandhari imetapakaa katika miundo kadha ya lugha: matamshi, fasihi, hadithi za kale, na kadhalika. Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika Mashariki kinafuatilia mbinu ambazo jamii tofauti hutumia kuzungumzia ardhi. Historia ya ukoo wangu iliyoanzisha utangulizi huu inaashiria jinsi ardhi, uhamiaji, na mandhari zimeathiri maisha ya wakaazi wa Afrika Mashariki. Safari na uhamiaji zimejaa katika ngano na sanaa ya jadi. Wahusika kwenye ngano hizi hueleza hisia tofauti tofauti—furaha, majonzi, au huzuni—wanaposimulia safari zao. Hivyo basi, busara ya kijamii—iliyokusanywa kwenye methali, vitendawili, mashairi, nyimbo, na hata riwaya—pia inaashiria hisia za aina nyingi mno. Kilicho cha umuhimu mkuu katika Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika Mashariki ni mazungumzo—aidha kwa njia ya mithili au la—ya mazingira katika fasihi.

Waandishi wengi wa fasihi ya Kiafrika wanavitumia vipengele vya mandhari kuashiria ujamaa, urafiki, au uhasama katika jamii. The River Between (1965) cha Ngũgĩ wa Thiong’o hutumia kukabiliana kwa milima miwili kuzungumzia mabadiliko ya kijamii yaliyowaathiri Wakenya katika enzi za mkoloni. Naye Chinua Achebe katika Anthills of the Savanna (1987) na Yvonne Vera katika The Stone Virgins (2002) huchunguza machungu yaliyojiri baada ya nchi za Kiafrika kupigania uhuru—hasa namna wanasiasa na viongozi walivyowadhulumu wananchi. Kunao uhusiano kati ya kichuguu faragha cha mchwa anachokichora Achebe na ugumu wa mawe unaoashiriwa katika kichwa cha riwaya yake Vera. Faragha na ugumu huu unatukumbusha serikali zao Sani Abacha (Nigeria), Mobutu Sese Seko (Zaire), Daniel Arap Moi (Kenya), na Hosni Mubarak (Misri), na jinsi utawala wao ulivyowanyima wananchi uhuru wa kupiga kura au kujiunga na siasa za upinzani. Kwa upande mwingine, Margaret Ogola katika The River and the Source (1994) anahimiza mwendo wa kasi ambao ni sifa kuu sio tu ya mito lakini pia ya vizazi vitatu vya wanawake ambao ni wahusika katika riwaya yake. Ngũgĩ, Achebe, Vera, na Ogola wanavitumia vipengele vya mandhari kuonyesha uhusiano katika jamii. Kunao pia waandishi wengi ambao wamepingana na unyanyasaji wa kisiasa kwa kutumia hali ya anga kama kiashiria cha upinzani. Kwa mfano, Coming of the Dry Season (1972) na Waiting for the Rain (1975) vya Charles Mungoshi huzungumzia vita vya uhuru huko Zimbabwe—Chimurenga—kwa lugha ya majira. Ukoloni ni msimu wa ukame, utakaotamatishwa na msimu wa mvua—au kujitawala kwa wananchi wa Zimbabwe.

Hatimaye, kunao waandishi ambao hupendekeza kujitawala kwa Waafrika kwa kutabiri uhuru hata kabla ya kuondoka kwa wabeberu. Jomo Kenyatta katika Facing Mount Kenya (1938), Alan Paton kwenye Cry, the Beloved Country (1948), nao J. M. Coetzee’s na A. P. Brink katika A Land Apart (1992) wamechangia hadithi ambazo zilitumiwa kuhamasisha vita vya uhuru. Kila kitabu kinatamani nchi huru ambazo—wakati vitabu vilipochapishwa—hazikuwa zimejiri. Ilhali Kenyatta na Paton wanayatamka waziwazi maneno Kenya na nchi katika vitabu vyao, The Promised Land (1966) cha Grace Ogot na A Farm Called Kishinev (2005) chake Marjorie Macgoye vinayategemea maneno “ardhi,” na “shamba.” Ogot na Macgoye husambaza fikra za mandhari ya Kenya ambazo zinaimudu fasihi kupingana na ukoloni wa Kiingereza.

Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika Mashariki linachambua jinsi mithili ya ardhi inatumika katika fasihi ya Afrika iliyotungwa kwenye karne za ishirini na ishirini na moja. Kazi hii ninaitekeleza kwa kuiga mbalamwezi. Umuhimu wa mahali katika historia za kijamii umefichwa peupe; kwa mfano, katika biografia niliyoanza nayo. Kwingineko, Carola Lentz anatatanisha tunavyoelewa mtazamo wa uhamiaji na wenyeji haswa wakati ardhi inatumiwa kuchangia uhasama wa kikabila. Kitabu chake Lentz, Land, Mobility, & Belonging in West Africa kinazungumzia jinsi wakaazi wa kwanza katika sehemu yeyote ile ni wahamiaji wa jadi kutoka sehemu nyingine. Wasomi wa Kiafrika wametia bidii kuielewa changa moto hii. Kazi hii haijakamilika. Kwenye sura za kitabu hichi, ninachambua riwaya, hadithi, na mchezo wa kuigiza ilikufuatilia jinsi fasihi huashiria ardhi na mandhari.

Mithili ya Mbalamwezi

Tofauti na jinsi falsafa ya “Enlightenment,” iliyowatenganisha binadamu kutoka kwa mazingira yao, mradi wangu katika kitabu hichi unasisitiza uhusiano mkuu kati ya watu na ikolojia. Ni kinyume cha mambo kwamba mfumo wa kiakili uliotafuta mbuni ya kuyaondoa mafundisho duni ya dini uliishia kuituza taji falsafa ya kiume iliyozaliwa bara la Ulaya na iliyokuwa ya daraja la juu, ya Kikristo, na iliyopingana katu na ushoga. Falsafa zingine zote ambazo hazikuambatana na hii zilikandamizwa, mara moja na kwa nguvu. Ardhi na Mandhari kinajaribu hasa kuufutilia utengano baina ya tamaduni na mazingira. Mbadala, ninachunguza aina mbali mbali za uhai—binadamu, mimea, na wanyama—pamoja na mazingaombwe. Usiku wa mbalamwezi, mwangaza ukimulika kote, binadamu, wanyama, na mimea hufanana miujiza. Vile vile topografia ambazo maisha haya yamejiezeka. Nilipowaza ni kwa njia gani Ardhi na Mandhari kinachangia uchambuzi wa fasihi ya Kiafrika, nilivutiwa na mithili ya mbalamwezi kuumulika ulimwengu. Mawazo kadhaa yamo katika mradi huu—ukoloni mamboleo, ikolojia, na hata usawa wa jinsia. Kitabu hiki kinazuru sehemu moja baada ya nyingine, kwa kuangalia hadithi moja kisha nyingine. Kwa haya yote, ninaikusanya miundo na mithili inayotumia ardhi na mandhari.

Mradi wangu unadondoa maana kwa kuunganisha fasihi ya Afrika Mashariki ambayo mara nyingi haisomwi pamoja. Katika uchambuzi wa fasihi hii, waandishi hawa hawapati kuongeleshana. Hoja ninayoifuatilia haijitokezi wazi wazi. Mbadala, maudhui yanadokezwadokezwa; mara yamefichika na mara yamo faraghani. Mjadala ambao ninajihusisha nao katika kitabu hiki una viashiria vichache. Ninategemea harufu, sauti, mtazamo, na mazungumzo ya wahusika ili kuelewa vyema mwelekeo wa vitabu na waandishi. Hizi ndizo ishara za utabiri na urambazaji ambazo ninanuia kufafanua katika sehemu kuu za Ardhi na Mandhari. Kwa ujumla, viashiria hivi vinaonyesha mithili ya ardhi, mandhari, wanyama, na topografia iliyotapakaa katika fasihi ya Afrika Mashariki. Katika vitabu hivi tunakumbana na mazingira ambayo yamegeuzwageuzwa. Sio hoja kwamba ardhi na mandhari yamefichika kivulini; aidha kwa kung’aa ama gizani, ardhi na mandhari yapo daima.

Ardhi kama Jinsia ya Kike

Katika shughuli tatu za ununuzi wa ardhi ambazo nimehudhuria, nilitambua kwamba ardhi ilibatizwa neno mbadala, “msichana.” Shughuli zote tatu zilitokea Oloitoktok, sehemu ya mashambani iliyo karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania. Kwa karne kadhaa zilizopita, Oloitoktok ilikuwa makazi na malisho ya jamii ya Wamasai. Hata hivyo, kuna historia kuu ya uhamiaji kati ya watu wa Kichagga, Kikuyu, na Kikamba katika eneo hili. Wakaazi huambatanisha uhamiaji wa hivi majuzi katika miaka ya Sitini, wakati familia za jamii ya Wakikuyu ziliwasili baada ya kuondokea ongezeko la idadi la watu katika mkoa wa Kati na kununua mashamba Oloitoktok.

Baba Njeri, ambaye nimejulishwa kwake na mamangu, ananisindikiza kukutana naye Baba Lekina. Baba Njeri anaanza kwa kusema “huyu kijana ameona msichana wako, na ana haja." Baba Njeri ndiye anayeniwakilisha; anazungumzia kuhusu matumaini yangu. Baada ya hapo, tunazungumzia bei ya shamba la ekari nusu ambalo Baba Lekina anauza. Huu ulikuwa mwaka wa 2017. Ilikuwa ni mara yangu ya pili kununua ardhi Oloitoktok. Na kama ilivyokuwa mara ya kwanza, mwaka wa 2016, ununuzi wa ardhi ulizungumziwa kutumia lugha ya ndoa. Mara hiyo ya kwanza, msemaji wangu alimuhimiza muuzaji asinidhulumu kibei kwa maana nikishanunua shamba hilo tutaanza kuishi kama mashemeji. Yaani, kubadilisha fedha na ardhi kulieleweka kwa lugha ile ile ambayo huambatana na mazungumzo ya mahari wakati wa ndoa. Miaka mitatu baadaye, David, rafiki wa karibu, anatutembelea nyumbani kwetu Oloitoktok. Anapumbazwa na mandhari ya Mlima Kilimanjaro. Anamuagiza babangu amjulishe kwa yeyote anayeuza shamba eneo hilo. Katika mazungumzo yanayofuata na Bwana James, babangu anaanza kwa kusema David amemwona na kumtamani “msichana” katika boma lake Bwana James.

Ni wazi kwamba mithili ya ardhi na mandhari imejaa katika lugha aina mbali mbali hapa Afrika Mashariki: fasihi, mazungumzo, ngano za jadi, na kadhalika. Ardhi na Mandhari kinafuatilia mawazo haya na kuchunguza jinsi jamii tofauti tofauti huzungumzia ardhi. Njia moja ya kuelewa mbona ardhi huchorwa kwa neno la msichana ni kutumia ubeberu wa Mwingereza. Kama wanavyosema Graham Huggan na Helen Tiffin, jamii zilizokuwa chini ya ukoloni zililumbikwa pamoja na mimea na wanyama, na baada ya muda jamii hizi zilishurutishwa kuyaazima maoni ya Ulaya kuhusu mazingira (6). Kunao uchunguzi mwafaka ambao huonyesha jinsi ukoloni wa nchi za Ulaya ulizichora miliki zao kama wanawake ambao walinajisiwa na wapelelezi wa kiume. Katika Postcolonial Ecocriticism: Literature, Animals, Environment, Huggan na Tiffin wanadai kwamba ukoloni mamboleo haujazorotesha mazingiria bali pia umedhoofisha falsafa ambazo Waafrika hutumia wanapozungumzia topografia zao, hasa ardhi (136-7). Kwa njia kuu, miili ya wanawake ilitumiwa kama viashiria vya ardhi iliyoshindaniwa na kumilikiwa na bara Ulaya (Loomba 154). Zaidi ya hapo walowezi wa kutoka Ulaya walisisitiza propaganda ambazo zilidharau mbinu jadi za ukulima za watu ambao mashamba yao yalinyakulia na mbeberu. Fasihi ya walowezi kama vile Robert Ruark, Isak Dinesen, Elspeth Huxley, Neil Sheraton, M. Harding, W. B. Thomas, M. M. Kaye, na C. T. Stoneham imejaa vijisababu vya kumnyima Mwafrika ardhi yake (Brown 117). Kitabu hiki kinauendeleza utafiti wa jinsi wakazi wa Afrika Mashariki hutumia ardhi, mandhari, na topografia katika mila, tamaduni, na ubinadamu wao.

Katikati ya mandhari ya kirasmi au ile ya kienyeji, ninaainisha mandhari hii ya mwisho kama mseto-kienyeji. Rob Nixon, kwenye, Slow Violence & the Environmentalism of the Poor, anazungumzia juu ya aina mbili ya mandhari: kienyeji na kirasmi. Nixon anaifafanua mandhari ya kienyeji kama ile iliyoundwa kwa kutumia ramani za kale ambazo vizazi kadhaa vimetunga; ramani hizi zina majina na mielekeo, na pia zina uhusiano mkuu na ikolojia na topografia ya sehemu fulani (17). Kwa upande mwingine, mandhari rasmi hutupilia mbali mbinu za jadi za kuijua mandhari. Kama wao Bill Ashcroft, Gareth Griffiths, na Helen Tiffin ninafafanua mandhari kama falsafa iliyo na msingi ambao hutenganisha dunia ya ukweli kutoka kwa kiumbe kinachoitazama (345). Kinachoibuka ni kulielewa neno “mahali” kama uhusiano tata kati ya lugha, historia, na mazingira (Ashcroft et al 345). Uhamiaji wa hivi majuzi wa jamii za Wakikuyu, Wakamba, na Wachagga katika eneo la Oloitoktok unapambana na mandhari ya kienyeji yaliyoundwa na jamii ya Wamasai. Wageni hawa hawasemi Kimasai na wameishi au kulima katika sehemu hizi kwa muda usiozidi vizazi viwili. Mizizi yao ni duni ikilinganishwa na wafugaji wenyeji wa eneo hili kwa karne kadhaa. Lakini hivyo sio kusema kwamba mandhari haya ya hivi majuzi ni rasmi. Mara nyingi, biashara ya mashamba haihifadhiwi wala kunakiliwa katika wizara za serikali. Na hata wakati pesa zinatolewa na mnunuzi na kupewa muuzaji hati ya umiliki haibadilishwi. Ingawa, kama Nixon anavyodai, wageni hapa Oloitoktok huichukulia ardhi hii kama ya kuchimbwa na kutumiwa kiholela, mandhari haya sio ya kirasmi, ya shirika lisilo la kiserikali, wala ya mashirika ya biashara za kimataifa (17). Wageni hawa wa hivi majuzi hawana nguvu za kiserikali au kiutawala ambazo huambatana na mandhari ya kirasmi. Lakini pia hawana ujuzi wa lugha, na desturi za jadi ambazo hushikilia mandhari ya kienyeji. Hata hivyo, kunao wageni au wakulima ambao huzungumza Kimasai, lakini hawa ni wachache sana.

Mbona Ardhi? Mandhari Inamaanisha Nini?

Katika mkusanyiko wa mila na desturi ambazo mtoto hupitia anapozaliwa, kujenga boma ni jambo la umuhimu sana nchini Kenya. Nyayo ambazo mtoto hufuata zinaandamana hivi: kuzaliwa; kujiunga na shule ya msingi; kufanya mtihani wa KCPE; kubaleghe; kujiunga na shule ya upili na kuufanya mtihani wa kidato cha nne; halafu kuhitimu na shahada ya kwanza. Kufunga ndoa na kununua ardhi—desturi ambazo husitiri maisha ya uchumi wa daraja la katikati—hufuatia miaka kadhaa ya kuajiriwa na kulipwa mshahara. Kuhamia nyumba mpya mara nyingi huadhimishwa kwa kuwaalika jamaa na marafiki katika karamu kubwa. Ardhi ni muhimu sio tu kwa kusaidia familia kujimudu kimaisha, lakini pia kwa jinsi ambavyo jamii hujitambulisha hadharani (Gertel eta l 1). Katika miaka ya kwanza kwenye karne ya ishirini, ardhi ilisitiri mizozo ya kisiasa iliyonuia kumtimua mbeberu. Ukabila ulipingwa, kama njia kuu ya kujitambulisha, wakati huo huo uraia wa Jamhuri ya Kenya ulizidi kutawala fikra za jamii mbali mbali. Kama Stuart Hall anavyotukumbusha, tabia na hisia za binadamu hubadilika daima (110). Ardhi na mandhari zilikuwa misingi nyeti kwa uundaji wa utu ambao ulizurura, ukahama, na ukajiunganisha na jamii au hata mataifa mbali mbali.

Ni vyema kusisitiza kazi maalum ambayo ardhi ilihitimisha kwenye siasa na uigizaji wa hekaheka za Mwafrika kujitawala. Amilcar Cabrar alizungumzia kwa upana umuhimu wa ardhi kwa Waafrika waliokuwa wakiwania uhuru. Cabral alihimiza ukombozi kamili wa ardhi na kazi ya mkono wake Mwafrika (62). Baada ya muda, ardhi lilikuwa neno lililosimamia maana nyingi na tofauti kwa wanasiasa na wanaharakati wa uhuru wa Mwafrika. Ilikuwa muhimu kwamba wakaazi wa bara la Afrika wamiliki ardhi sio tu ya kujipa shibe, lakini pia ya kujengea uhusiano na raia wenzao.

Ardhi Katika Vita Vya Uhuru

Wanasiasa ambao huifuata falsafa ya Karl Marx, kama vile Cabral, husisitiza mno juu ya uchumi wa kisiasa. Kunazo sababu mwafaka za kufanya hivyo. Kama vile Marxism, Modernity, & Postcolonial Studies kinavyodai, haiwezekani kutofautianisha maisha ya kila siku kutoka kwa maswali nyeti kuhusu uchumi wa nchi (Bartolovich 6). Katika karne iliyopita, uchunguzi wa nchi za Kiafrika baada ya mwisho wa ukoloni umejaribu kuzingatia namna ardhi na mandhari yalishambuliwa katika lengo lake mkoloni kuuhimiza ubepari (Lazarus 11). Desturi za Waafrika ambazo hazikuambatana na ubepari zilivunjwa, zikadhoofisha, na mwishowe zikafanywa haramu (Lazarus 11). Naye Robert Marzec anazungumzia tamaduni za ubeberu zilizokuwa viguzo vya uchumi wa kikoloni (11). Kwa njia hiyo hiyo, ili kuondoa ukoloni, inabidi kuzipambua mbinu zake mkoloni za kuzalisha uchumi na utamaduni.

Mwanaharakati Franz Fanon alipendekeza kwamba jambo la umuhimu kabisa katika kuuangamiza ukoloni lilikuwa Waafrika kumiliki ardhi yao wenyewe. Fanon alizingatia ardhi kama namna ya kujipa mkate wa kila siku na pia kuusitiri utu (44). Homi Bhabha na Edward Said wanazingatia mada ile ile. Hatimaye, ni muhimu kujikumbusha kwamba ukoloni, kama vile vita, ni mbinu mojawapo ya kunyakua ardhi.

Ardhi Katika Falsafa ya Kuondoa Ukoloni

On Decoloniality huunganisha nadharia na matendo. Walter Mignolo na Catherine Walsh wanasisitiza kwamba nadharia ni kutenda, na kutenda ni nadharia (7). Yaani, elimu na upinzani huambatana. Falsafa hii imetekelezwa na msemo kufikiria-kutenda na kutenda-kufikiria katika kuangamiza ukoloni (Mignolo & Walsh 9). Kwa sababu hii, ngano zina umuhimu mkuu katika kuwahamasisha raia juu ya siasa za ukombozi. Kama vile mabeberu walivyotunga hadithi za kusaidia ukoloni vivyo hivyo wananchi wa nchi mbali mbali walianzisha vita vyao katika sehemu ya utamaduni. Ukoloni ulivunja sio tu ardhi za Waafrika, lakini pia tamaduni zao na historia zao (Deane 10). Vita vya ukombozi hung’ang’ania ardhi na dini na jadi ambazo mkoloni alidunisha (Cesaire 43). Katika Darker Side of Western Modernity, Mignolo anaelezea swala hili kama ukoloni wa nyakati na mahali (21). Sera ambazo zilinyakua ardhi ya Mwafrika zinapatikana katika nchi tofauti tofauti kama vile Afrika Kusini, Algeria, Kenya, na Zimbabwe. Na kama tulivyoshuhudia katika miongo sita iliyopita, changamoto za ugawaji ardhi zimezidi tangu nchi hizi kujiwania uhuru.

Katika lengo la kuuangamiza ukoloni, Ardhi na Mandhari kinafafanua nyakati na mahala kwa njia tofauti. Ilhali ninachunguza fasihi iliyochapishwa kati ya miaka ya 1966 na 2014, mazungumzo yangu yameelekezwa na historia ya nchi za Afrika Mashariki. Pia ninazingatia kuwepo kwa harakati za kibiashara, kielimu, kijeshi, na kidini kutoka wakaazi wa bara la Ulaya. Uchambuzi wa riwaya zao Nyeko, Ogot, Ogola, Owuor, Vassanji na wengineo, umejengwa kwenye msingi wa karne moja unusu ya historia ya jamii za Afrika Mashariki. Niliichagua njia hii ili kutatanisha mawazo ya kawaida kuhusu nchi za Kiafrika. Vyombo vya habari katika nchi za Magharibi hupuuza mara nyingi uhusiano uliopo kati ya ukoloni mamboleo na ubeberu wa hapo awali. Ni nadra sana kuona wanahabari hawa wakizungumzia historia ya miaka elfu moja kabla ya kuwasili kwa mzungu katika bara Afrika. Kitabu hiki kinaangazia mipaka iliyotungwa na wakoloni; mara kwa mara ninaipuuza mipaka hii ili kufuatilia tabia za kikabila na kiraia. Ninazimulika siasa za ukombozi ambazo zilianzishwa na jamii mbali mbali aidha kupinga ukoloni au ukoloni mamboleo.

Katika Ardhi na Mandhari kuna umuhimu mkubwa wa kuichunguza historia ambayo vitabu hivi vimetungiwa. Zaidi ya hapo, ninatilia maanani jinsi waandishi wanavyoitumia historia; jinsi mambo yaliyopita yanavyoathiri maisha ya sasa. Kwa kweli, teleolojia ya nyakati—inayoandamana moja kwa moja kuelekea ustaarabu wa Ulaya na Amerika Kaskazini—inafaa kuchunguzwa zaidi. Zaidi ya harakati za kuuondoa ukoloni, mazungumzo kuhusu ardhi na mandhari wakati dunia imekumbwa na mabadiliko makuu yasiyorekebishwa katika hali ya hewa yanatubidi kuangazia sehemu kubwa zaidi za wakati na mahali (Clark, Ecocriticism on the Edge 13). Kuisoma fasihi ya Afrika Mashariki iliyoandikwa baada ya miaka ya Sitini ni kuangalia, wakati huo huo, ukoloni wa tangu karne ya kumi na tisa na pia mabadiliko ya tabianchi tangu mapinduzi ya viwanda. Hili sio swala la mzaha.

Kuyaelewa mabadiliko ya hali ya anga kunamaanisha pia kuvitatua vyombo vya usasa katika nchi za magharibi: busara ya kimantiki iliyosisitiza kuugawanya ulimwengu kwa vipande viwili viwili. Mafafanuzi haya hujitokeza kama uainishaji wa vinyume: mwanamke/mwanamume, binadamu/mnyama, asili/ustaarabu, na pia mweusi/mweupe. Lakini juhudi za kuyaelewa mabadiliko ya hali ya hewa hayawezi kufuatiliwa kwa kutumia falsafa hizi hizi. Inatubidi tuubadilishe mtazamo wetu wa nyakati na mahali (Clark, Ecocriticism on the Edge 22). Yaani, hatuwezi yaendesha mambo kama kawaida. Kwa mfano, mtazamo wake Robert Marzec kuhusu unyakuzi wa ardhi katika nchi za Ulaya na kilimo-biashara katika nchi zilizokuwa chini ya ukoloni (11). Vile vile, mawazo yake Mike Davis kwamba katika miaka hamsini ambayo baa la njaa nyakati za amani lilitokomea ndiyo muda ambao baa la njaa liliongezeka kwa kiwango kikubwa katika sehemu zote zilizokuwa chini ya ukoloni (9). Njaa ilizuka kokote mkoloni alijinyakulia na njaa ndiyo ikawa sababu kubwa ya mbeberu kujinyakulia ardhi ya Mwafrika.

Kwa sababu hizi, inafaa tuchunguze kwa umakini jinsi tunavyofafanua mambo kadha kama vile mila, desturi, asili ya ukoo, na hata utu au ubinadamu (Clark, Ecocriticism on the Edge 20). Vitengo hivi vyote vimetatizwa mara kwa mara. Kwa mfano, raia waliokuwa chini ya ukoloni walidhaniwa kuwa kama wanyama pori. Kwa vile wageni wa Ulaya hawakuzitambua sheria zao, bunge zao, dini zao, sherehe na faraja zao, au hata mbinu za kusambazia habari waliyaona duni maisha yao kwa ujumla. Ikiwa hivyo, lengo langu katika Ardhi na Mandhari ni kuzifikiria upya mbinu za kuashiria mandhari ambayo yanapendeza; haswa, nina hamu kuzungumzia sehemu ambazo zinaikiuka mipaka ya nchi huru na kuizingatia, mbadala, dunia nzima (Heise 10). Sense of Place & Sense of Planet: The Environmental Imagination of the Global linatuhimiza kushuhudia mabadiliko ya hali ya hewa kwa njia kuu ambayo inazingatia sio tu jinsi ukoloni ulivyodhoofisha mazingira tofauti tofauti, lakini namna raia walijisitiri dhidi ya mabadiliko haya na pia kuichora topografia yao. Jinsi jamii hizi zilivyoashiria mandhari yao kunaweza kutusaidia katika kuzielewa changamoto za leo kama vile utawala, siasa, udikteta, na hata njia za kuuangamiza ukoloni na ukoloni mamboleo.

Katika kitabu hichi, ninanuia kuzifafanua siasa za kuashiria mandhari. Kazi hii ninaitimiza wakati wa mabadiliko makuu ya hali ya anga,, lakini pia dunia nzima inapokumbwa na jangwa la COVID-19, serikali mbali mbali zinazowadhulumu raia, kudhoofika kwa ushiriki wa raia katika mipangilio ya demokrasia, na uongezekaji wa Ufashisti na ubaguzi wa rangi katika nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, na hata chuki dhidi ya wageni huko Uchina na Afrika Kusini. Lengo langu ni kuepuka changamoto za kale na kung’amua mafunzo yeyote ambayo tunaweza tukayatumia kusonga mbele. Akizungumzia ukatili wa polepole, Rob Nixon anawaza juu ya mbinu mbali mbali za kuashiria mabadiliko ya ikolojia ambayo huchukua muda kabla ya binadamu kuyaelewa (3). Vurugu hii isiyo kasi imechangia sio tu katika kudhoofika kwa hali ya anga lakini pia katika kufifia kwa falsafa za kienyeji. Uharibifu wa historia, busara, mila, na tamaduni za jadi umechangia pakubwa katika uharibifu wa mazingira. Ardhi na Mandhari kinaonyesha kwamba waandishi wa Afrika Mashariki wamezungumzia mambo haya sambamba angalao kwa muda wa miaka hamsini na pengine kwa muda mrefu zaidi. Fasihi ya nchi hizi, katika mtazamo wa ukoloni duniani kote, tayari imegundua mbinu za kuashiria vurugu ya taratibu ambayo haina wahusika wakuu na ambayo vyombo vya habari hupuuza (Nixon 3). Uchambuzi wangu unaeneza utafiti wa ikolojia kutumia falsafa zinazozingatia ukoloni mamboleo. Chemi chemi ya utafiti huu inatambulika kwenye picha za mazingira ambazo waandishi hutumia katika tungo zao za sanii.

Zaidi ya kujishughulisha na kwa nini ardhi na mandhari zinapatikana katika fasihi, pia nina hamu ya kutambua vipi ardhi na mandhari zinatumiwa. Mwandishi anachagua vipi jinsi atakavyotumia ardhi na mandhari katika kitabu chake? Fasihi inaweza onyesha kilicho-kweli-lakini-hakitambuliki na pia kile-ambacho-hakijavumbuliwa. Hapo awali nilionyesha jinsi Kenyatta na Paton waliweza kubuni nchi ambazo, na uraia ambao, bado haukubuniwa. Waandishi wa Afrika Mashariki walitunga harakati za ukombozi ambazo zilizaa utawala wa Mwafrika. Vile vile, sanaa tofauti tofauti zinaonyesha uharibifu wa mazingira ambao mara nyingi unapuuzwa. Changamoto za kuashiria ambazo Clark anazungumzia zinatatuliwa na wasanii ambao huisaidia umma kuelewa tishio ambazo hazitambuliki aidha kwa sababu ni kubwa/kidogo zaidi, au zinatokea mbali sana nasi, au zinachukua muda mrefu zaidi ya maisha ya binadamu anayetazama (Nixon 15). Nixon anasisitiza kwamba ni rahisi sana kupuuza maafa ya hali ya anga hasa yanapotukia kwa watu wengine ambao sio majirani wetu. Lakini wakati janga linapotukumba sisi, nyumbani, mahitaji ya kila siku—yakihimizwa na ubepari—yanatuelekeza kinyume na suluhisho zozote: hamna kutafakari, lakini mna uraibu.

Fasihi inayohamasisha ina uwezo wa kumulika uharibifu wa mazingira kwa njia ambayo inaeleweka kwa urahisi (Nixon 15). Ni muhimu kuzingatia mithili na hila za riwaya, pamoja na hitimisho zozote ambazo mwandishi anatunga. Ardhi na Mandhari kinapanua namna tunavyofafanua “uhai” kuwahusisha pia wanyama, mimea, na viumbe hadubini. Uchambuzi wangu unaashiria jinsi topografia ilivyo na wakala wa kuhitimisha mambo kadha. Ninayapanua maswali yake Cheryll Glotfelty: waandishi wanayachoraje mazingira; waandishi wanatumia vipi ikolojia katika riwaya; ni busara gani ya jadi ambayo imo kwenye hadithi; ni mithili gani za ardhi ambazo zimetumika; mwandishi anaashiriaje misitu na vichaka (xix)?

Misitu ya Kissidougou, Afrika Magharibi, ni mfano mwafaka wa swala hili. Wageni kutoka Conakry hutembea sehemu hii iliyoko Kusini Mashariki mwa Guinea na kujiangalilia vichaka. Wakaazi wa miji mikuu, maafisa wa serikali, na hata makarani wa ukoloni wameshindwa kuelewa mazingira ya Kissidougou. Aidha kwa sababu matembezi yao hufanywa msimu mmoja na sio mwingine, kuwadharau wanakijiji, au kwa juhudi za kufaidi kibiashara, watalii hawa huona uharibifu wa mazingira hata ingawa macho yao yanawadanganya (Fairhead & Leach, 268-9). Hii ni kufuatia desturi ya wakoloni kudai kwamba wenyeji wa jadi katika eneo la Kissidougou wamedhoofisha misitu na kuikata bila mpangilio (Fairhead & Leach 268). Lakini ukweli ni kwamba, wenyeji ndio ambao wameipanda miti na misitu ile ile ambayo wanashtakiwa kwamba wamekata (Fairhead & Leach 2). Sio wana-Kissidougou ambao wameikata misitu ya jadi iliyokuwepo, mbadala, hapakuwepo misitu hapo awali na wakulima hawa ndio wameipanda misitu hii na kuitunza. Utawala wa mkoloni wa kuidondoa rasilimali ya Mwafrika, pamoja na serikali huru za Guinea-Conakry ambazo zinaadhiriwa na ufisadi ndiko kumechangia katika kuwadunisha wana-Kissidougou kama watu wanaoharibu mazingira.

Kissidougou ni mfano mwafaka kwamba nafasi ina maana nyingi tofauti; nafasi haitekelezwi kwenye eneo la jiografia pekee, lakini pia kijamii na katika tamaduni (Darian-Smith, Gunner, & Nuttall 2). Njia hizi mbali mbali za kuimudu nafasi zinachangia katika uchambuzi wangu wa fasihi ya Afrika Mashariki na jinsi waandishi wanaashiria ardhi, mandhari, mahali, na nafasi. Mandhari ni dhana inayogusia historia, upinzani wa tamaduni, pamoja na maana tofauti za ardhi na mahali (Darian-Smith, Gunner, & Nuttall 3). Ingawa vitabu viwili au vitatu ninavyozungumzia katika Ardhi na Mandhari vinaashiria ardhi na mandhari kwa umbali, hiyo si hoja. Kama Different Shades of Green kinavyotukumbusha, ni muhimu kutenganisha ukoloni, usasa, ubeberu, na mabadiliko ya hali ya anga. Mambo haya yanachangiana. Kama nilivyoonyesha hapo awali, uharibifu wa busara za kienyeji kuhusu mazingira kumechangia pakubwa katika unyakuaji wa rasilimali za bara la Afrika, aidha msituni, mtoni, ziwani, baharini, shambani, au mgodini.

Inafaa nifafanue jinsi ninavyoyatumia maneno “nafasi” na “mahali” katika kitabu hiki, hasa katika mwelekeo wa kuumaliza ukoloni. Neno mahali lina maana za kijiografia, kimazingira, na hata kinasaba (DeLoughrey & Handley 4). Kumbu kumbu ya ukoo wangu iliyoanzisha utangulizi huu inaonyesha jinsi mahali na kiini cha jamii vinachangiana. Mahali ni dhana tata inayohusisha hisia sio tu za kimwili lakini pia za kiakili na kiroho. Kuna pengo kubwa kati ya uzoefu wetu wa mahali na jinsi lugha inavyomudu mahali katika sanaa (Ashcroft, Griffith, & Tiffins 9). Jinsi waandishi wa Afrika Mashariki wanavyobuni lugha ambayo itachora ardhi, mandhari, na topografia kunachangia pakubwa katika harakati za riwaya kuumaliza unyanyasaji.

Kitabu hiki kinachunguza jinsi binadamu huwadhulumu wanyama na jinsi binadamu huwanyanyasa wenzao wanyonge (Mwangi 2). Mimea na wanyama ni mifano ya maisha ambayo ina nguvu za kuumba. Ndovu ni mfano mzuri wa jambo hili: Ndovu hufyeka nyika, huangusha miti, na kuunda vijia vinavyoelekea mtoni na kwa hivyo huwasaidia wanyama wengine wa porini kupata malisho. Ndovu wa msituni hula matunda yaliyoanguka na kuziangusha mbegu katika kinyezi, ambacho huchangia miti kuota. (Orenstein 17) Jinsi tunavyompendelea binadamu hutufanya kuyadharau matendo ya mifano mingine ya maisha hapa duniani. Na hata katika riwaya, tunavyoashiria mimea na wanyama kunachangia ubora na ukubwa wa binadamu. Katika enzi za mkoloni kuliibuka sayansi na teknolojia ambayo ilitumiwa sio tu kutawala mimea lakini pia kuwadhulumu watu (Oslund 2).

Petals of Blood na Unyakuzi wa Ardhi

Fasihi yake Ngũgĩ wa Thiong’o imechangia pakubwa katika kuupinga ukoloni mamboleo. Ngũgĩ amezingatia swala la unyakuzi wa mashamba kupitia falsafa za Kisoshalisti tangu miaka ya Sabini. Wahusika katika hadithi zake wamenyimwa ardhi-ambayo hapo awali ilitunukia hisia za jamii. Kwa sababu hiyo wahusika hawa huungana na walala hoi wenzao au wafanya kazi wengine ili kuanzisha upinzani dhidi ya ubepari. Katika Petals of Blood, Ngũgĩ anaangazia jinsi mkoloni alivyonyakua ardhi, kisha mifugo, akidai mali hii ni kodi dhidi ya jamii ambazo zilipigana na mabeberu; baadaye, mkoloni alikamata vijana na kuwalazimisha kufanya kazi shambani (18). Zaidi ya hapo, wanakijiji wanahofia biashara ya mzungu kwa maana bado wanakumbuka jinsi mkoloni alivyochukua ardhi yao, jasho lao, na mali yao na kuwarudishia sarafu ambazo hazingelika, huku akidai hiyo ndiyo mali halisi (Ngũgĩ 18).

Ngũgĩ pia anaonyesha shaka dhidi ya ubepari duniani na juhudi mbali mbali za maendeleo, hasa katika nchi za Afrika na bara Hindi. Kwa kuiga lugha ya magazeti, Ngũgĩ anawapa wasomaji tangazo la vifo vya wanabiashara watatu katika mji mdogo wa Ilmorog—mahali ambapo matukio katika hadithi hii yanafanyika. Tangazo hilo linawafananisha wanasiasa wa Jamhuri ya Kenya na wapelelezi wa karne ya kumi na tisa ambao walizihudumia nchi za Ulaya. Ngũgĩ anafanya mzaha kwa kudai kwamba vifo vya matajiri hawa watatu vinawasononesha mno raia. Hii ni kwa maana wanaume hawa walikiinua kijiji cha Ilmorog kwa kujenga viwanda vikubwa vikubwa ambavyo vimekuza uchumi wa sehemu hii (Ngũgĩ 5). Mwandishi anaunganisha unyakuzi wa ardhi katika enzi za mkoloni na miradi ya maendeleo na unyanyasaji wa mafukara mikononi mwa wanasiasa wa Kiafrika. Kama vile wakoloni waliamua jinsi rasilimali ya nchi itakavyogawanyishwa ndivyo wanasiasa wanajinyakulia mali ya uma kwa mbinu za ufisadi. Katika sehemu hii ya riwaya yake, Ngũgĩ anaonyesha jinsi teknolojia ya ukoloni iliyaharibu mazingira ya nchi za Afrika. Hapo zamani: Ardhi haikununuliwa wala kuuzwa. Mashamba yalikuwa mengi, na yalitumiwa kujimudu kimaisha. Kwa vile ardhi ilipatikana kwa urahisi, haikuwa hoja kukilima kijishamba kimoja mwaka baada ya mwaka. Nchi yote ilizingirwa na misitu. Miti hii ilivutia mvua, na kufanya kivuli. Lakini gari la moshi liliiharibu misitu. (Ngũgĩ 82) Petals of Blood kinapinga uchumi wa wakoloni ambao ulitegemea utumizi mbaya wa rasilimali. Cha kuhuzunisha ni kwamba serikali huru barani Afrika ziliendeleza mfumo huu wa maendeleo. Kwa kufanya hivyo, serikali hizi zilidunisha ndoto za raia za kuijenga nchi yao kwenye misingi ya haki na usawa. Zaidi ya hapo, Ngũgĩ anaishitumu sana dini ya Kikristo; anazungumzia Utatu Mtakatifu wa Bibilia, Sarafu, na Bunduki (88).

Unyakuzi wa ardhi ulikuwa tukio lenye huzuni nyingi kwa jamii, kwa maana wananchi walipoteza sio tu njia ya kujimudu kifedha lakini pia mbinu za kujitawala kisiasa. Wahusika wake Ngũgĩ wanasononeka kwamba hapo awali walikuwa na uhuru wa kuyachagua maisha yao. Walitunga nyimbo zao na kucheza ngoma watakavyo. Lakini uhuru huu ulinyakuliwa mikononi mwao (115). Ngũgĩ anatumia mithili ya nyimbo—mifano mikubwa ya tamaduni za Afrika—kuashiria utawala wa kisiasa kabla ya kuwasili kwa mabeberu. Kwa kufanya hivi, mwandishi anasisitiza namna jamii za jadi zilijitawala. Baada ya ukoloni kuanza, Waafrika waliimba lakini nyimbo zilitungwa na wageni wa Ulaya; hii ni tofauti sana na enzi za kale ambako Ilmorog, na hata bara nzima la Afrika, lilijitawala (Ngũgĩ 115; 125). Munira, mhusika ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, anaisimulia historia ya Bw. Mwafrika: Leo nitawaeleza historia ya Bw. Mwafrika katika sentensi tatu. Hapo zamani, alikuwa na ardhi na akili na roho. Siku ya pili, mabeberu waliuchukua mwili wake na kuuza. Siku ya tatu, baada ya kuona kwamba anapigana, walileta mapadri na walimu ili kuifunga akili na roho yake ndivyo wageni hawa wakaweza kuinyakua ardhi yake kwa urahisi. (236) Ni kwa uchungu wakazi wa Ilmorog wanautazama usaliti wa viongozi wao. Baada ya kuwa na imani kwamba maisha yatabadilika baada ya kujiwania uhuru, wahusika wake Ngũgĩ wanafadhaika kwamba hata ingawa Mwafrika mwenzao anaitawala nchi, ubepari bado upo. Jamhuri ya Kenya ni sehemu ambayo uhodhi bado umeenea. Walalahoi hawana wa kuwashughulikia. Ngũgĩ anazungumzia Kenya mpya kama mahala ambapo hamna cha bure. Bila pesa huwezi pata ardhi; na bila ardhi au mali huwezi ukapata mkopo wa benki kuanzisha biashara au kununua ardhi (254). Hata baada ya uhuru, ardhi ndiyo njia kuu ya kujiendeleza kiuchumi; kwa bahati mbaya umiliki wa ardhi bado umewekewa vikwazo vingi. Zaidi ya hapo, tatizo lingine ni kwamba historia yake Munira imempuuza Bi. Mwafrika. Ngũgĩ anaibuni historia ambayo inawazingatia wanaume pekee. Wanawake hawamo katika hadithi hii ya mali, upinzani, na kunyanyaswa ambayo Mwalimu Munira anasimulia.

Maendeleo ya kiuchumi ambayo yametokea baada ya uhuru, hasa uongezekaji wa viwanda, umeyadhoofisha maisha ya wenyeji hapa Ilmorog. Watu hapa wanaishi katika madongo poromoka; wamekanishwa kuingia wilaya za mabwanyenye ambazo hapo awali ziliishi wakoloni wa Ulaya (302). Lengo lake Ngũgĩ katika Petals of Blood ni kuangazia jinsi jamii huyabadilisha mazingira yao. Ngũgĩ ni mmoja wa waandishi ambao hujaribu kuyakomboa mandhari ya Kiafrika kwa niaba ya wenyeji (Loflin 76). Ardhi na Mandhari kinapanua wazo hili kwa kuvichambua vitabu kwa waandishi ambao hawana umaarufu mwingi, na pia kwa kuonyesha jinsi mada hii inaendelezwa katika fasihi ya karne ya ishirini na moja. Ulumbikaji wa mali unasababisha mawazo mazito. Kama anavyouliza Ngũgĩ, kwa nini ardhi, ambayo ni urithi wa raia wote wa Jamhuri ya Kenya, ikamilikiwa na mtu binafsi? Kenya, ni shamba la wananchi wote (302). Hapa pana upinzani kati ya nia au faida za kibinafsi na mahitaji ya jamii kwa ujumla. Ilhali wakazi wa Ilmorog, na wafanya kazi pamoja na wakulima wanaiona rasilimali ya nchi kama ya kutumiwa na umma, kunao viongozi ambao wameteka nyara utawala ili kukusanya mali haramu kwa njia za ufisadi.

Ardhi na Mandhari pia kinanuia kuzielewa mbinu za usanii ambazo waandishi hutumia. Ninachunguza kama uchoraji picha za mandhari ambazo zinapuuza unyanyasaji wa kisiasa kunazuia kitabu fulani au riwaya fulani kutimiza lengo lake la kukabiliana na ukoloni. Kwa mfano, katika Petals of Blood, ingawa Munira anatizama wanakijiji kama wameungana kimaisha na udongo wao, wazo hili linapuuza ugumu wa ukulima katika sehemu ya Ilmorog (Ngũgĩ 24; 75). Ingawa kuna mandhari ya kupendeza mno, pia kuna hofu nyingi. Safu ya milima, ikishuka kuelekea mto Ilmorog, ni mandhari ya kuvutia mno kote duniani (Ngũgĩ 67). Hata hivyo, kuna mdudu anayeharibu maua, na kufanya yasizae matunda; kwa hivyo, wakati Munira anadai kwamba lazima jamii iangamize wadudu anazungumuzia sio tu ukulima, lakini pia watekelezaji wa ukoloni mambo leo—wadudu ambao wameharibu matunda ya uhuru (Ngũgĩ 22). Ngũgĩ anadai kwamba maisha vijijini hayajaboreshwa tangu nchi ijiwanie uhuru; ukweli ni kwamba kwa njia moja au nyingine hali ya wakulima wadogo imezorota. Kuzidunisha ndoto za raia ni kosa kubwa ambalo viongozi wa nchi huru wamefanya.

Tayari kuna uchambuzi mkubwa wa fasihi yake Ngũgĩ ambao umefanywa na wasomi kame vile Simon Gikandi, Evan Mwangi, Gῖchingiri Ndῖgῖrῖgῖ, na James Ogude. Mukoma wa Ngũgĩ ameangazia waandishi wengine wa enzi za Makerere. Hata hivyo hakuna utafiti mwingi ambao umeangalia waandishi wa kike waliochapisha riwaya katika miaka ya Sitini. Ardhi na Mandhari kinanuia kumtizama Grace Ogot. Samba samba na vitabu vyake Ngũgĩ Weep Not, Child (1964), The River Between (1965), na A Grain of Wheat (1967), The Promised Land (1966) chake Ogot kiliendeleza siasa za kuupinga ukoloni. Ilhali mada zao Ngũgĩ na Ogot zinaambatana, Ogot hajakaribishwa katika ukumbi wa fasihi ya Afrika Mashariki kama alivyotukuzwa Ngũgĩ. Katika sura ya kwanza ya Ardhi na Mandhari ninachambua hadithi yake Ogot. Kama mwandishi wa kwanza wa kike kuchapisha kitabu Afrika Mashariki, Ogot anafaa kutukuzwa zaidi.

Ni Kwa Nini Mazungumzo Haya Yanafaa Kwa Wakati Huu?

Jinsi maoni potofu kuhusu ardhi ya bara la Afrika yanavyodumu kunafanya Ardhi na Mandhari kuwa na umuhimu mkuu wakati huu. Uwongo kuhusu idadi kuu ya mashamba huru kumevutia mabeberu tangu karne ya kumi na tisa (Cotula 8). Hivi leo, nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini zinaendelea kuinyakua ardhi ya Waafrika ili kuzalisha utajiri—mafuta ya kuendesha magari, mali ya kumudu wafanyakazi wastaafu, na njia za kuokoa nishati bila kupunguza njia za matumizi (Cotula 174). Kimsingi, kuna mkabiliano kati ya ardhi kama mbinu ya uwekezaji—kama inavyobuniwa na fedha za kigeni—na ardhi kama chanzo cha ujamaa na tamaduni—kama wanadhania wenyeji wa sehemu mbali mbali.

Katika The Great African Land Grab Lorenzo Cotula anadai kwamba upungufu huu umesababishwa na wanasiasa pamoja na wanasheria. Serikali za kikoloni na pia zile za nchi huru ziliuza ardhi na kwa sababu hiyo hivi leo tunashuhudia kuzorota kwa ardhi kama msingi wa mahusiano ya ujamaa (Cotula 176). Fasihi inauliza maswali nyeti kuhusu ununuzi, ubadilishaji, na umiliki wa ardhi. Kunazo tofauti kadhaa wakati mwandishi anazingatia ardhi na mandhari katika riwaya yake. Kwa mfano, Petals of Blood na The Great African Land Grab vinahitimisha mada moja: kwamba swala kuu katika utetezi wa ardhi barani la Afrika ni kuhusu umiliki—nani ana nguvu na uwezo wa kubadili sera zinazohusika na ardhi (Cotula 181). Kama anavyosema Abdon Rwegasira katika Land as a Human Right: A History of Land Law & Practice in Tanzania, ardhi sio muhimu tu katika kujimudu kimaisha, kulima shibe, na kufuga wanyama, lakini pia kama chanzo cha uhasama katika mahakama ambako kuna washindi na walioshindwa (xx).

Ardhi na Mandhari Katika Fasihi ya Afrika Mashariki ni muhimu kwa wakati huu; ni cha kuogofya kwamba hivi leo bara la Afrika linavamiwa mara nyengine na wageni ambao wanatamani ardhi yetu. Kama unyakuzi wa hapo awali, unyakuzi wa karne ya ishirini na moja pia utaathiri maisha ya Waafrika. Kuna nchi nyingi za kigeni ambazo zimekimbia kujinyakulia rasilimali hapa Afrika. Kwa mfano ujenzi wa mabarabara na reli nchini Ethiopia, Kenya, na Nigeria na kampuni za Kichina; kukodisha mashamba makubwa huko Tanzania na kampuni za Malaysia ambapo wanapanda na kuvuna nishati ya mimea; na kampuni za Qatar zinaendeleza kilimo biashara huko Kenya. Zaidi ya hapo, kuna majeshi wa wanamaji wa kutoka Marekani, Uchina, na Ufaransa ambao wamefanya kambi nchini Djibouti, pamoja na ngome za Unmanned Aerial Vehicles huko Niger. Ingawa hizi juhudi zinapangwa kama kinga dhidi ya magaidi, huu pia ni upinzani wa kidunia kati ya Marekani na Uchina. Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umekataza halmashauri za kimataifa kukodisha mashamba makubwa huko Afrika Magharibi na kupanda vyakula. Kwa sababu hiyo, changamoto la wakulima wadogo kupoteza ardhi yao limetwaaliwa na wanahabari wa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini kama swala nyeti la wakati huu—ambalo lina wahalifu wanaojulikana (nchi za bara Hindi na Uarabuni) na wahasiriwa wanaotambulika (Waafrika wanyonge). Ardhi na Mandhari kinanuia kuyatatua maswala haya kwa kutumia ujuzi wa fasihi, kisiasa, kiuchumi, na hata ikolojia.

Muhtasari wa Sura

Katika sura ya kwanza, “Settlers, Lands, & Landscapes: Presence of Nonhuman Life,” ninachambua The Promised Land (1966) chake Grace Ogot sambamba na The River and the Source (1994) chake Margaret Ogola. Utafiti wangu unaonyesha jinsi waandishi hawa wawili wanapingana na falsafa ya ubeberu. Mabeberu walitazama mazingira ya Afrika Mashariki kwa kuondoa mimea, wanyama, na mazingaombwe ambayo wenyeji walitilia maanani na ambayo ni mifano ya uhai uliokuwepo mbele ya binadamu yeyote kuishi sehemu hizi. Ilhali ramani, picha, na propaganda za mabeberu zilisaidia unyakuzi wa ardhi, Ogot na Ogola wanaonyesha pia jinsi siasa za mabeberu ziliunganishwa pamoja na vita dhidi ya Waafrika. Hadithi zao zinatatanisha riwaya ya uhalisi na kuonyesha jinsi uhasama uliathiri mandhari na raia waliokuwa chini ya utawala wa mkoloni. Ogot, kwa kuhadithia safari ya familia moja kutoka nyumbani kwao hadi ugenini, anapingana dhidi ya unyakuzi wa ardhi iliyodhaniwa kuwa pweke na kuwafaa Wazungu. Vivyo hivyo, Ogola, anatumia hadithi za jadi kuashiria mandhari ambayo yanategemea umiliki wa vizazi kadhaa. Akoko, nyanya shupavu na ambaye ni mhusika mkuu katika riwaya yake Ogola, anasimulia hadithi za Kiluo na kuambatanisha hadithi hizi na makazi ya jamii hii katika magharibi mwa Kenya. Kwa mfano, wilaya kama Gem, Sakwa, na Rachuonyo zina majina sawia na mashujaa ambao wamo katika hadithi zake Akoko.

“Land & Landscape in Zimbabwean Narratives of Trauma,” sura ya pili, kinachambua fasihi yake Yvonne Vera kando na waandishi wengine wa Zimbabwe ambao wana mwelekeo wa uhalisi na utaifa. Ilhali Vera anapendelea simulizi ya sauti nyingi na utumizi wa mithili katika riwaya zake, waandishi wenza wanabuni njama zinazofuatana moja kwa moja. Waandishi kama vile Solomon Mustwairo, S. Nyamfukudza, na Charles Mungoshi wanapingana na ubeberu huko Afrika kusini kwa kutumia wahusika wanaokomaa kimaisha na kiakili, jinsi nchi ya Zimbabwe ilivyoondokea utotoni wa mkoloni na kuingia utu uzima wa kujitawala. Kwa upande mwingine, waandishi kama A. Kanengoni na Yvonne Vera hukana ubeberu wa mzungu kwa kutumia hadithi zenye jamii ya wahusika wengi. Kwa kuwabuni wasimulizi wengi—ambao husema hadithi zao kwa njia ya mviringo—waandishi hawa wawili wanatoa changamoto kwa mtazamo wa mandhari ya Zimbabwe ambao unapuuza vita na pia usimulizi wa historia ya Zimbabwe ambao unaangazia mashujaa na kuwapuuza raia wa kawaida. Vitabu vyake Vera, kwa mfano, vinahimiza uraia wa Kizimbabwe ambao ni huru na wenye nguvu. Ushairi wake Vera katika The Stone Virgins (2002) unahusisha fahamu ya jamii nzima. Kuashiria ujasiri wa wahusika wake wa kike, Vera anafuma sauti za usimulizi ambazo zinajumuisha wazazi, wapenzi, wakulima wadogo, wanyama wa pori, misitu, na wakongwe wa vita vya Chimurenga. Hii ni busara ambayo inakanusha, kwa nguvu, falsafa za maendeleo na usasa, aidha zinazotokona na mabeberu wa karne ya ishirini au utaifa wa watu weusi baada ya miaka ya sitini.

Sura ya tatu, “Belonging & Mobility: Representations of Urban Landscapes,” inachunguza riwaya za mijini zilizoandikwa na Mkenya, Marjorie O. Macgoye, na Mtanzania, Moyez G. Vassanji. Sehemu hii inadai kwamba raia hukiuka amri ili kuashiria umiliki wa ardhi. Uchambuzi wangu unatofautiana na utafiti wa hapo awali kwa kuzingatia miji sio tu kwa mada za kitamaduni lakini pia kwa swala za kijiografia. Wakazi wa miji hukabiliana na vipengele hivi viwili kwa ukiukaji sheria wa kimakusudi. Ninapozungumzia Coming to Birth (1986) ninaonyesha jinsi Marjorie Macgoye anabuni wahusika wa kike ambao hukiuka sheria na pia kufanya uigizaji wa kila siku. Kwa mfano, mhusika mkuu anaashiria makazi yake katika jiji la Nairobi kwa uigizaji; Ardhi na Mandhari kinadai kwamba wakazi wa Nairobi hukiuka mipaka na vikwazo ambavyo vimewekwa ili kuwanyima uhuru, hasa wa mienendo. Kwa njia hii, wao husisitiza kupenya kwenye zile zile sehemu ambazo wamekatazwa kuingia. Sehemu ya mwisho ya sura hii inazungumzia Uhuru Street (1991) kilichoandikwa na M. G. Vassanji. Riwaya yake Vassanji inadai kwamba lazima tuzingatie sehemu za umma pamoja na zile za kibinafsi kama eneo za kisiasa ambazo zinashuhudia mng’ang’anio wa utawala. Yaani sehemu za kijiografia pia huathiri migogoro ya kisiasa; jiografia aidha ndiyo chanzo cha mgogoro au ndio jukwaa ambalo huchezewa vita hivi. Hatimaye, kwa kuangalia changamoto zinazoikumba jamii ya Wahindi inayoishi Afrika Mashariki, Vassanji analipatia swala la ukabila kipaumbele na pia kuonyesha jinsi vita vya kisiasa au vya kitamaduni vinaweza kuathiri jiografia tofauti tofauti.

“African Languages, African Socialisms, & Representations of Lands & Landscapes,” sura ya nne, inazungumza kuhusu Mhabeshi Berhane M. Sahle Sellassie na Mtanzania Ebrahim Hussein kuonyesha jinsi siasa za lugha na fasihi ya Kiafrika zinaathiri viashiria vya ardhi na mandhari. Ebrahim Hussein katika Arusi (1980) anasimulia jinsi Tanzania ilivyoangamiza ukoloni lakini ikaishia ukoloni mamboleo. Tamthilia yake Hussein inaonyesha jinsi ubinafsi ulivyodhoofisha ujamaa. Kwa jumla, vitabu vyake Hussein ni mfano mzuri wa changa moto ambazo waandishi wa lugha za Kiafrika wanapambana nazo. Katika The Afersata (1968), B. M. Sahle Sellassie anazipinga siasa duni zilizozuka baada ya miaka ya sitini. The Afersata kinaashiria manufaa ya ujamaa. Kwenye riwaya hii, kibanda kinachoteketea moto, kubomoka, na kuwa majivu ni mithili ya makazi pamoja na mandhari ya Kihabeshi (Sahle Sellassie 3). The Afersata kama Arusi kinahukumu serikali kwa kuwanyanyasa raia na kutoweza kuanzisha sera za haki na usawa. Mwishowe, The Afersata kinazungumzia mandhari kwa lugha ya uumbaji na uharibifu ambayo inafanana na usemi wa kisiasa katika nchi ya Uhabeshi. Kama yeye Hussein, Sahle Sellassie analiangazia swali la lugha—hata kwa kuchapisha riwaya katika lugha ya Gurage, inayozungumzwa Uhabeshi kusini.

Sura ya mwisho katika Ardhi na Mandhari inachunguza jinsi binadamu wanaathiri ikolojia, na pia namna ikolojia inawaathiri binadamu katika riwaya za Yvonne A. Owuor (Kenya) na Monica Arac de Nyeko (Uganda). “Representations of Lands & Landscapes at the Humanity-Ecology Interface” kinadai kwamba hadithi zao Nyeko na Owuor—ingawa zimeandikwa nyakati na mahali tofauti—zinaonyesha namna uharibifu wa mazingira huambatana na uhasama dhidi ya wanawake na raia wanyonge. Katika Dust (2014), Owuor anauchora mviringo wa maisha na kifo katika eneo za Kenya kaskazini. Sehemu ya mwisho ya sura hii inazichambua hadithi fupi za Nyeko; kuna faida tatu za kufanya hivi. Hadithi hizi zinaangazia wahusika wa kike katika viashiria vya ardhi na mandhari na kuonyesha mbona madai ya ardhi huambatana mara nyingi na ukabila. Kwa hivyo, hadithi hizi ni mifano mwafaka ya fasihi kama mbinu ya upinzani, na zinatuwezesha kuchunguza ukatili dhidi ya miili ya wanawake. Hatimaye, hadithi yake “Banana Eater” (2008) inafichua jinsia na ukabila katika mandhari za mijini.

Katika hitimisho langu, ninazungumzia kwa ufupi manufaa ya kutumia lugha za Kiafrika katika usomi wa bara la Afrika na hasa fasihi. Ninaonyesha faida za njia hii hasa: kuzirudia busara za kiasili. Manufaa mengine ni kuzigeuza mbinu za kisasa za utafiti wa maswala ya Kiafrika ambazo hupendelea Kizungu, Kifaransa, na lugha zingine za kigeni ilhali zinatenga Kiswahili, Kikuyu, Kizulu, Kiyoruba, na lugha nyingine za kiasili.